Somalia inakiuka haki za wafungwa - HRW

wafungwa hawana haki Somalia
Shirika la kutetea haki za binadamu Human rights watch limeishutumu serikali ya Somalia kwa kuwanyima wafungwa haki za uakilishi wa wakili na kuwashitaki raia wa kawaida chini ya mahakama za kijeshi.
Shirika hilo limesema kuwa mamia ya raia wanahukumiwa kwa sheria kali wasizoelewa. Human rights watch pia imesema kuwa raia wengi wamejikuta matatani baada ya kukamatwa katika msako wa kitaifa unaofanywa na mashirika ya kijasusi ya Somalia na mara nyingie wanazuiliwa kwa muda mrefu bila kufunguiwa mashtaka.
Kuzuiliwa kwa muda mrefu ni tatizo ndogo sana kwa raia hao wa Somalia ikilinganishwa na kufunguliwa mashtaka ya ugaidi na kutishia usalama wa nchi. Ukipatikana na hatia, hukumu ni kifo.
Licha ya kuwa mashirika ya haki za binadamu yamekuwa yakipinga kutolewa hukumu hii, Somalia ni mojawepo ya nchi chache Afrika ambayo bado inatoa huku hiyo.
Wasiwasi mkubwa ni kwamba, washukiwa hawapewi fursa ya kujitetea. Na wala mahakama hizi za kijeshi hazihitaji ushahidi mwingi kuamua kuwa una hatia.
Human rights Watch imetaja katika ripoti yao kisa kimoja ambapo zaidi ya kesi 24 zilisikilizwa na kuamuliwa kwa chini ya siku 4.
Mahakama yajitetea
Lakini akijibu madai hayo, mwenye kiti wa mahakama za kijeshi wa Somalia Liban Cali Yarow ameambia BBC kuwa ni upuuzi mtupu na mwingilio wa jamii ya kimataifa katika mambo yasiyowahusu.
''Haya mashirika ni ya nje, na hayajui mambo yanayofanyika nchini kwetu. Inasikitisha kwamba hawazungumzii matatizo yetu ila wanapiga kelele tunapojaribu kujitatulia wenyewe. Ripoti hiyo imejaa madai yasiyo kweli.''
Human rights watch iliwahoji zaidi ya watu 30 na familia za watu walio shutumiwa, na wengi wao wamesema kuwa mahakama hizo haziwapi wafungwa nafasi ya kujitetea.
Mara nyingine hata kuwalazimisha kukiri mashtaka ambayo hawakufanya na hakuna ruhusa ya kukata rufaa. Hapa ndipo mwisho wa kesi.
Jamii ya kimataifa

Sasa shirika hilo limetoa wito kwa jamii ya kimataifa na hasa wafadhili kushinikiza Somalia kurejesha haki za wafungwa na kuzuia raia kushtakiwa katika mahakama za kijeshi.
Lakini mwenyekiti wa mahakama hiyo Liban Cali Yarow amepuuzilia mbali ripoti ya shirika hilo akisema kuwa imejaa madai ya uongo.
''Ningependa kumsihi yeyote ambaye ana malalamiko juu yetu awasilishe kwetu badala ya kuandika kwenye magazeti. Kuandika tu bila kutushauri ni sawa na kutuwekelea madai ya uongo.'' Amesema Liban Yarow.
Maafisa wa Somalia wametetea hatua ya kuwashtaki washukiwa wa ugaidi katika mahakama za kijeshi wakisema kuwa mahakama za kiraia hazina ulinzi wa kutosha na uwezo wa kusikiliza kesi zenye uzito mkubwa kiasi hicho
Previous
Next Post »